Saturday, 21 June 2014

Mkojo, mbegu za kiume zinapotokea kwenye paja

Paja la mguu wa kushoto wa Hubert Mkenda (49) mkazi wa Kijiji cha Msaranga, Kata ya Kitale, Rombo mkoani Kilimanjaro, limetoboka na kutengeneza sehemu ambayo inapitisha haja ndogo (mkojo) na mbegu za kiume.

Mkenda ambaye ni baba wa watoto saba amekuwa katika hali ya ugonjwa kwa miaka 11 sasa na jitihada za madaktari wa Hospitali za KCMC Moshi na Huruma iliyopo Rombo mkoani humo, hazijamwezesha kuondokana na maumivu makali ambayo yanatokana na tundu hilo.

Tiba ya mwisho aliyoipata ni pale madaktari wa KCMC walipomwekea mpira kwenye nyonga kwa ajili ya kuwezesha kutoa mkojo, lakini wakati mwingine umekuwa ukitoka kupitia kwenye paja na kumsababishia maumivu makali.

“Ninapata maumivu makali mkojo unapopita kwenye paja na ninapokuwa na hisia za mapenzi, mbegu za kiume hupita kwenye shimo lililotoboka kwenye paja,” anasema Mkenda na kuongeza:

“Ni vigumu kueleza maumivu tabu na shida zinazoniandama, maisha yangu yamebadilika ni kama Mungu amechoka kusikia kilio changu lakini bado naamini ananipenda,” ni maneno ya uchungu anayoyasema Mkenda huku akionekana kukata tamaa na kuongea:

Anaendelea: “2003 ni mwaka ninaotamani usingekuwepo kabisa duniani  kwakuwa ni mwaka uliobadilisha maisha yangu na kunifanya kuwa mteja wakuhudhuria  hospitali kila siku bila matumaini”.

Mkenda alipata ajali ya gari 2003 katika msitu wa Rongai na kujeruhiwa vibaya katika maeneo ya haja kubwa na haja ndogo, ajali ambayo imesababisha kulazwa hospitalini kwa miaka 5 mfululizo na kufanyiwa upasuaji kwa nyakati tofauti mara nane.

Ajali ilivyotokea

Mkenda anasema hakumbuki siku, lakini ulikuwa mwezi Julai 2003, alipoondoka nyumbani kwenda Rongai kufanya kibarua cha kuvuna mahindi kwenye shamba la mtu na alipomaliza kuvuna akiwa na wenzake walipakia mahindi kwenye gari na kuanza safari ya kurejea Mashati, Rombo.

Anasema njiani dereva wa lori walimokuwa wamepakia mahindi, alisimama na kupakia magogo ya miti, kisha kuendelea na safari, lakini wakiwa njiani moja ya gogo lililokuwa limetoka nje ya gari liligonga kwenye mti na kumrusha juu.

“Nilirushwa juu na kutoka huko nilianguka chini kwa kishindo na kukalia gogo kisha kurushwa nje ya gari na kuangukia mti, niliumia vibaya sehemu za haja kubwa na ndogo,” anasimulia Mkenda.

Mkenda anasema alikimbizwa katika Kituo cha Afya Tarakea alikopewa huduma ya kwanza, lakini kutokana na kuvuja damu nyingi sehemu ya haja kubwa, walishauri akimbizwe katika Hospitali ya Huruma.

“Pale Huruma walinitundikia chupa ya maji na damu na kuniweka kwenye gari la wagonjwa na kunipeleka KCMC, ambako madaktari walibaini kwamba mti uliingia sehemu ya haja kubwa na kunijeruhi vibaya,” anaongeza.

Anasema akiwa KCMC ambako alilazwa kwa mwezi mzima, alifanyiwa upasuaji tumboni na kuwekewa mpira wa haja kubwa kisha kuruhusiwa kwenda nyumbani, huku akiambiwa arejee hospitalini hapo baadaye.

Hata hivyo kutokana na hali yake, hakuweza kuhimili kuishi katika mazingira ya nyumbani kwake, hivyo alichukuliwa na hospitali ya Huruma, ambako aliendelea kuishi chini ya uangalizi wa madaktari.

Anasema baada ya miezi minne madaktari wa Huruma walifanikiwa kufunga sehemu ambayo alifanyiwa upasuaji na kuwekewa mpira kwa ajili ya kutoa haja kubwa, hatua ambaye ilimwezesha kutoa haja kubwa kwa njia ya kawaida.

Mkenda anasema hata hivyo baadaye aligundua tatizo lingine la haja ndogo kutokea njia ya haja kubwa. “Madaktari wa Huruma walinifanyia upasuaji ili kulikabili tatizo hili, lakini walishindwa hivyo walinipeleka tena KCMC ambako pia madaktari walinifanyia upasuaji mwingine,” anasema Mkenda na kuongeza:

“Waliniwekea mpira wa mkojo na nilitakiwa kurudi nyumbani kusubiri ujio wa madaktari bingwa ili wanifanyie uchunguzi zaidi, kwahiyo badala ya kwenda nyumbani nilirudi palepale hospitali ya Huruma ambako nilikaa muda mrefu kama miaka mitatu hivi”.

Mkojo kutokea pajani

Mkenda anasema wakati akiendelea kusubiri madaktari bingwa, mwaka 2006 alipata matatizo miguu yote miwili kujikunja pamoja na kutokwa na vidonda sehemu mbalimbali za mwishi.

“Madaktari walisema hali hii ilitokana na kulala kwa muda mrefu na walinishauri nirudi tena KCMC kutibiwa miguu iliyokuwa imejikunja na pia mguu wa kushoto ulianza kuviba hasa sehemu ya paja,” anasimulia. Anasema wakati akiwa KCMC kusubiri kunyooshwa miguu aligundua kuwa kuwapo kwa tundu kwenye sehemu ya paja ya mguu wake wa kushoto, ambalo lilikuwa likipitisha mkojo hivyo aliwajulisha madaktari.

“Mwanzo madaktari hawakuamini kama mkojo unapita kwenye paja, niliwambia wasubiri waone, hivyo walinisimamisha na mkojo ulitoka kwa kasi, kiasi kwamba uliwachafulia nguo walizovaa, ndipo walipoamini kuwa ni kweli mkojo unatoka kwenye shimo lililotokea lenyewe kwenye paja,”anasema Mkenda.

Anasema hali hiyo iliwafanya madaktari wamrudishe kwenye chumba cha upasuaji ili kufahamu tatizo na kugundua kwamba mguu huo ulikuwa na usaha, hivyo waliuondoa na mkojo ulirejea kutoka kupitia kwenye haja kubwa.

Anasema madaktari bingwa walifanya tena upasuaji na kufanikiwa kurudisha mkojo kwenye njia yake ya kawaida lakini uzima huo ulidumu kwa siku sita na ukurudi kutoka kwenye shimo lililochimbika kwenye paja.

Mkenda anasema kutokana na hali hiyo, madaktari walimfanyia upasuaji chini ya nyonga na kupitisha mpira wa mkojo anaoutumia mpaka sasa na kwamba madaktari walisema wameshindwa kujua tatizo.

Kunyooshwa miguu

Baada ya matibabu ya mkojo kushindikana, Mkenda anasema  madaktari wa KCMC walimsaidia kunyoosha miguu yake kwa kwa kumfunga POP huku akiendelea kulazwa hospitali hapo kwa mwaka mmoja na nusu, lakini hatimaye miguu ilinyooka.

Anasema mara baada ya miguu kunyooka alipatiwa magongo ya kutembelea kwani mguu unaopitisha mkojo na mbegu za kiume ulikuwa kama umepooza.

“Maisha yake yamekuwa ya hospitalini zaidi na hata sasa madaktari wameniambia wazi kwamba hawana uwezo wa kunitibu tena, labda nikatibiwe nje ya nchi, pia wamenishauri kwamba ninywe maji mengi ili mkojo utoke msafi, usiniunguze hapa kwenye paja,” anaeleza Mkenda.

Mkenda anasema hana ndugu wakumsaidia katika matatizo aliyonayo, kutokana na familia yake kumtelekeza na kwamba tangu alipopata ajali na maisha yake yamekuwa yakumtegemea mkewe ambaye pia ni mama wa nyumbani.

Anasema madaktari wamemshauri kama anauwezo akatibiwe nchini India jambo ambalo kwake ni mtihani mwingine maishani mwake, kutokana na ugumu wa maisha.

Mkenda anawaomba watanzania wenye mapenzi mema kumsaidia ili aweze kwenda nchini India ambako gharama halisi za tiba ni Sh15 Milioni.

“Nawaomba wale wenye mapenzi mema, Watanzania wenzangu wanisaidie maana nataabika, nina akauti Benki ya NMB namba 40310022192 au MPESA kupitia namba 0759 38 01 66.

Mkewe na watoto

Josepha Elibarik ambaye ni mke wa Mkenda, anasema baada ya mumewe kupata ajali maisha yamekuwa magumu kwakuwa yeye amechukua nafasi ya baba na mama nyumbani.

“Mwandishi mimi ni mama wa nyumbani, nijue mgonjwa anaishije bado watoto wanahitaji kwenda shule na kula ni maisha magumu sana lakini namshukuru Mungu,”anasema Josepha.

Mama huyo anasema kutokana na ajali ya mumewe watoto wake wawili walishindwa kuendelea elimu ya msingi na badala yake waliacha na kuanza kufanya kazi mbalimbali ili kusaidiana naye kuendesha maisha ya familia.

Picha ya Hubert Mkenda akionyesha miguu ilivyokuwa imekunjika, kabla madaktari wa KCMC kufanikiwa kuirejesha katika hali yake ya kawaida. Via Mwananchi