Thursday, 3 April 2014

Unayenunua maziwa ya kopo Supermarket angalia usije ukaumia. Mfuate vitendo hapa kwa mengi juu ya hili.

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imefungia maduka makubwa (Supermarket) 39, yakidaiwa kuuza vyakula hatarishi kwa afya na uhai wa binadamu.

Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, amesema miongoni mwa bidhaa zilizokutwa katika maduka hayo kupitia operesheni iliyoendeshwa kati ya Machi 10 na 20 mwaka huu, ni maziwa ya kopo, chumvi na vinywaji vya kuongeza nguvu.

Bidhaa katika maduka hayo, baadhi yake zilibainika kuwa bandia, zisizo na ubora. Nyingine zilikutwa zikiwa na vifungashio vilivyoandikwa lugha ya kigeni, isiyoeleweka kwa walaji wengi.

Alitaja majina ya baadhi ya maduka husika yaliyoko jijini Dar es Salaam, na kusema sheria itachukua mkondo wake kuhakikisha inakuwa mfano.

Kwa upande wa maziwa ya kopo, taarifa ya mkurugenzi huyo kwa waandishi wa habari, inasema yamekamatwa 591 yenye thamani ya Sh milioni 17 na utaratibu wa kuyaharibu unaandaliwa.

Alitaja majina ya maziwa hayo ni SMA 1, 2 and 3, Promol Gold, S-26 Gold, Nursoy, Progress Gold, Cow & Gate, Isomil 2, InfacareSoya, Nutrikids na Aptimil 1.

“Maziwa hayo pamoja na kuwa hayajasajiliwa, lakini pia yalifungwa kwenye vifungashio vyenye lugha isiyoeleweka na ingawa uchunguzi unaonesha lugha hiyo ni kichina. Hiyo ni kinyume cha sheria ya vifungashio vya vyakula inayohimiza vyakula vyote kuambatana na maelekezo kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza zinazoeleweka kwa walaji wengi,” alisema.

Alitaja bidhaa nyingine zilizokamatwa kwenye kwenye operesheni iliyoendeshwa kati ya Machi 10 na 20 mwaka huu, jijini Dar es Salaam, ni vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini makopo 1,526.

Vinywaji hivyo ni aina ya Monster, B52, Krazy, Relentless, Boost, Red bull toleo la red, Silver na Blue, Rockstar, Climax na Atlas vyenye thamani ya Sh milioni 4.5.

Aidha TFDA imekamata paketi 6,090 za chumvi zenye thamani ya Sh milioni tano; ikidaiwa kuwa bandia.

Alitaja majina yaliyo kwenye paketi hizo ni Lo Salt, American Garden Salt, Kensalt, Saxa, Chilly Willy Salt, Today’s Essential, Best Salt Nezo Salt, DP na Costa Salt ambazo pia zinasubiri kuharibiwa kwa mujibu wa sheria