Jumla ya meno ya tembo 495
yamekamatwa kwenye maeneo
mbalimbali nchini katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.
Aidha watuhumiwa wa ujangili 544
wamefunguliwa mashitaka kwenye
mahakama mbalimbali ambapo kesi 62 zimemalizika huku 38 zikiwa bado zinaendelea.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Paul Sarakikya, alibainisha hayo mjini hapa jana alipokuwa akitoa taarifa ya robo mwaka juu ya hali ya ujangili
nchini.
Alisema kuwa nyara hizo za serikali
zilikamatwa kutokana na doria
iliyoendeshwa na watumishi wao waliopo kwenye mapori ya akiba na kikosi cha kuzuia ujangili kwenye maeneo mbalimbali.
Sarakikya alisema kuwa katika kipindi hicho, jumla ya mizoga ya tembo 39 ilionekana ndani na nje ya hifadhi za taifa na mapori ya akiba huku nyama za wanyamapori kilo 1,111 zikikamtwa.
“Aidha meno ya tembo yaliyokamatwa yalikuwa katika hali mbalimbali ambapo mazima yalikuwa 171, vipande 22 vya
meno ya tembo ghafi, vipande 302 vya meno ya tembo yaliyochakatwa yenye jumla ya kilo 662.62 yalikamatwa,” alisema.
Alisema kuwa pia walifanikiwa kukamata silaha 11 ikiwemo bunduki ya rasharasha 1, rifle 3, shotgun 2, gobore 5 pamoja na
risasi saba za aina mbalimbali.
“Mali na vifaa vingine vilivyokamatwa ni pamoja na magari matano ambavyo
vilikamatwa kwa kuhusika kwenye
vitendo vya ujangili hasa wa meno ya tembo, ng’ombe 2,663 walioingia kwenye hifadhi pamoja na msumeno mmoja wa kukata mbao na mbao 745,” alisema
Sarakikya.
Alisema kati ya kesi 124 zilizofunguliwa kwenye mahakama tofauti nchini, 62 zilizokuwa na washitakiwa 85 zilimalizika kwa watuhumiwa kulipa faini ya zaidi ya sh milioni 25.5.
Sarakikya alisema meno ya tembo
waliyokamata yalitokana na matukio ya siku za nyuma, jambo alilodai walilibaini kutokana na meno hayo kuwa yamebadilika rangi kwa kuchimbiwa ardhini muda mrefu huku mengine
yakimeguka.
Taarifa hii imekuja siku moja baada ya watu sita wanaodhaniwa kuwa ni majangili kukamatwa na meno ya tembo 53 yenye jumla ya kilo 169.7 wakiwa na silaha aina ya SMG yenye magazine tatu kwenye Kijiji cha Kiomboi wilayani
Manyoni mkoani Singida.